Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumilla ni mji wenye takribani wakazi 27,000 ulioko kusini mashariki mwa Uhispania. Hapo awali, chama cha mrengo wa kulia nchini Uhispania kilipendekeza bungeni kupiga marufuku kila aina ya mikusanyiko ya kidini kwenye viwanja vya michezo na maeneo mengine yanayofanana, na baadaye pendekezo hilo likaidhinishwa na chama cha mrengo wa katikati cha Uhispania ambacho meya alikuwa mwanachama wake.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mikusanyiko yote ya kidini na kitamaduni ya kigeni katika viwanja vyote vya michezo na maeneo yanayofanana ilikuwa ni kinyume cha sheria, na cha kusikitisha ni kwamba waathirika wa mwanzo wa kupitishwa kwa sheria hiyo walikuwa ni Waislamu wa Jumilla.
Tukitazama historia ya nchi hii, tunaona kwamba kwa karne nyingi Uhispania ilikuwa ikitawaliwa na Waislamu, na athari zake zinaonekana katika lugha ya Kihispania na pia katika vivutio maarufu vya utalii wa nchi hiyo, vikiwemo Kasri maarufu la Kimoori la Granada.
Kwa bahati mbaya, serikali za mrengo wa kulia uliokithiri katika baadhi ya maeneo ya Ulaya, huchukua hatua za kupitisha sheria zinazopiga marufuku mikusanyiko ya kidini. Mwaka uliopita kosa hili lilikaririwa katika mji mmoja wa Italia na meya wake wa mrengo wa kulia uliokithiri, ambapo alitangaza marufuku ya kuswali swala ya jamaa, jambo lililozua upinzani kwa Waislamu 8,000 wa mji huo na kumfungulia mashtaka mahakamani.
Chanzo: Euro News
Maoni yako